CCM Inawachimbia kaburi Wabunge Wake

Na Happiness Katabazi

WANAFALSAFA wa masuala ya sayansi ya jamii, wanaamini kuwa nyakati zinafundisha binadamu kufikiri na kutenda kulingana na mahitaji ya watu na mabadiliko.

Kwa nini wanafalsafa hao wanadhani na kufikiri hivyo? Wanaamini kwamba ushujaa wa jana, waweza ukaonekana kuwa ufisadi leo.

Nayasema haya kutokana na mwenendo wa Bunge letu la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma, dhidi ya mwenendo wa kiongozi wa serikali bungeni, Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba.

Kwa nafasi yake Lowassa, kama kiongozi wa serikali bungeni anayetokana na chama tawala cha CCM, amekuwa akiwaita wabunge wa chama chake na kukaa kama kamati kwa lengo la kuwafunda kila linapotokea tatizo linaloonyesha udhaifu ndani ya serikali.

Lowassa na Makamba, Jumamosi iliyopita waliongoza kikao cha wabunge wa CCM kwa lengo la kufanya tathmini ya mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha.

Katika kikao hicho, wabunge wa CCM wanadaiwa kuzibwa midomo ili wasiikosoe serikali kwenye vikao vya Bunge kwani ukosoaji huo eti unamkera Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Kikao hicho kilitawaliwa na mazungumzo ya kuwatisha wabunge wa CCM ambao walikosoa bajeti ya mwaka 2007/2008 wazi wazi.

Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, alitishia kuondoa shilingi katika mshahara wa Waziri Mkuu kwa kutoonekana kwa baadhi ya barabara katika bajeti ya mwaka huu ambazo zimeainishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha unaoishia Juni mwaka huu.

Akichangia hotuba ya Wizara ya Fedha katika majadiliano yanayoendelea bungeni, Selelii alisema katika bajeti ya awamu iliyopita barabara hizo ziliainishwa, lakini kwenye bajeti ya awamu hii hazionekani.

Akiwa amekwisha kutamka kuwa na mwongozo wa Mungu katika mchango wake huo, mbali na kutamka nia yake ya kutoa shilingi katika mshahara wa Waziri Mkuu, Selelii pia alizishambulia Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Miundombinu kuwa mipango yake kwa mwaka 2007/2008, hairidhishi. Nako alitishia kuondoa shilingi.

Hata hivyo alisema analazimika kukubaliana na bajeti hiyo kwa shingo upande kwa kuwa hana jinsi ya kuipinga kutokana na kubanwa na ilani ya uchaguzi ya chama chake.
Inawezekana kabisa kwamba CCM inafanya hivyo kwa nia njema kabisa, lakini, kwetu sisi tulioko nje na ambao ni wengi na tuliowatuma wabunge wetu kusema hayo wanayodadisi, hatuwezi kuwa na tafsiri nyingine juu ya mwenendo huo wa kufinya sauti ya umma.

Katika mfumo wa demokrasia ya uwakilishi, jamii inawategemea wabunge wao wakawasemee yale wanayohitaji kwa ajili ya maendeleo yao na pia yanayowakwaza, bungeni.

Katika mfumo wa demokrasia ya uwakilishi, jamii inategemea kusikia hoja za wawakilishi wao zikipatiwa majibu sahihi kutoka katika serikali yao ambayo wao ndio wameiweka madarakani.

Kinyume cha hapo kama serikali itataka kila inachokisema na inachokitaka kipite tu bila vikwazo, tena kwa lazima, basi hilo halitakuwa jumuiko la Bunge kwa maana ya mkusanyiko wa watu waliofikishwa huko kwa njia ya demokrasia.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba ‘ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo na wala haujali adui wala rafiki.’

Ieleweke nayaandika haya si kwa kuwachukia Lowassa, Makamba au kiongozi yeyote yule wa serikali anayeingilia uhuru wa maoni ya wabunge wetu. Nasisitiza mawazo ya wabunge wetu lazima yaheshimiwe.

Tunasema hivyo kwa sababu serikali, kama serikali inaweza isiyajue mahitaji halisi au wananchi na hivyo hata mipango yake ikawa ni ya mbali sana na wananchi.
Lakini wabunge kama wawakilishi wa wananchi, wanaishi nao na hivyo wanayajua mahitaji na vipaumbele vya wananchi.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alikuwa kiongozi wa shughuli za serikali bungeni pekee kwa kipindi cha miaka kumi ambaye alimudu vyema kufanya kazi yake bila ya kuitisha vikao vya falagha kuwafunga midomo wabunge ambao walikuwa wakiichambua serikali.

Sote tutakumbuka Bunge la mwaka 1995-2000 lilikuwa na idadi kubwa ya wabunge wa kambi ya upinzani kama kina Ndimara Tigambagwe, James Mbatia, Dk. Masumbuko Lamwai, Mabere Marando, Agustine Mrema na wengine, hakika walilichachafya Bunge na serikali.
Lakini kamwe hatukuwahi kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba Sumaye alikuwa akifanya pilikapilika za kuitisha vikao na kutumia mbinu za kuwaziba midogo.

Sasa ajabu tunayoiona hivi leo ambapo ndani ya Bunge kuna idadi ndogo ya wabunge wa upinzani lakini tunashuhudia wabunge wakiminywa sauti zao.

Narejea kauli ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) mapema mwaka huu alidiriki kusema wazi wazi kwamba serikali imekuwa kikwazo cha demokrasia ndani ya Bunge. Hakika hii si sifa nzuri hata kidogo.

Hatari ninayoiona hapa ni kwamba endapo CCM itaendelea na utaratibu wake huo wa kuwakusanya wabunge wa CCM, na kuwafunda pindi wanapoonekana kuibana serikali, basi itambue ajira za wabunge zitakuwa shakani katika uchaguzi ujao.

Inachokifanya CCM leo ni sawa na kuwachimbia kaburi wananchi, kwani hawataeleweka kwamba chama kimeweka msimamo wa kutohoji kushindwa kutekelezwa kwa baadhi ya miradi na ahadi za wakati wa kampeni.

Kwa vyovyote vile, ipo siku watasimama na kumhoji mbunge wao aliyesimama ndani ya Bunge, akatoa hoja zake nzito za utetezi wa wananchi wake hadi povu likamtoka mdomoni, lakini akaishia kupitisha bajeti ya wizara kwa asilimia 100 wakati hatapewa majibu ya hoja zake.

Ikifika hapo, ajue ajira yake hiyo ya kisiasa, itakuwa halali kwa kambi ya wapinzani kwa kuwa jamii kwa ujumla na wapinzani wa kisiasa wa mbunge husika wa ndani na nje ya chama chake, wanamsikia na kumpima kwa umakini mkubwa sana.

Kwa bahati nzuri sana, hivi sasa Watanzania wengi wameamka.Yote haya yanayotendeka ndani ya Bunge na yote yanayofanywa na viongozi wa CCM, wanayatambua. Wanaweza wasiyaseme leo, lakini 2010 hawatakaa kimya.

katabazihappy@yahoo.com; www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis.Juni 28,2007

3 comments:

  1. Hii wala haina shaka kabisaaaa!! Watu walishaanza kuelewa, ipo siku mambo yatakuwa vingine!

    Asante sana Katabazi!

    ReplyDelete
  2. ni kweli wabunge wa ccm wanaandaliwa mazingira magumu sana mara watakapoenda kuomba kura mwaka 2010,mf mbunge mmoja alisema bungeni "wapiga kura wangu wamenipigia simu wakisema nikatae bajeti ya wizara ya fedha" lakini kinyume na matarajio yangu mwishoni aliunga mkono bageti 100% bila kujibiwa hoja zake kwa kuofia kiboko kutoka kwa Makamba na Waziri mkuu. kazi yako ni nzuri endelea kutujulisha na zaidi fuatilia habari za BoT kwa ajili ya faida ya watanzania sasa na wakati ujao

    ReplyDelete
  3. dada nimepitia blog yao hii
    umejitaidi sanaaa.. Nikiwa admin
    wa www.haki-hakingowi.blogspot.com
    ntafanya juu chini kuitangaza blog yako hiiii kwa manufaa ya jamiii
    nzimaa...
    Nakutakia kila la kheri
    haki.yako@gmail.com

    ReplyDelete