MWANAMKE WA SHOKA JESHI LA POLISI TANZANIA


KUTANA NA MWANAMKE WA SHOKA JESHINI…
Sydney Mkumbi:
Mwanamke ‘mzito’ pekee Jeshi la Polisi
.Ndiye aliyeongoza kumhoji Abdallah Zombe
.Ni bosi kitengo cha makosa dhidi ya binadamu

KUTANA na mwanamke wa kwanza ndani ya Jeshi la Polisi anayeongoza Kitengo cha Makosa dhidi ya Binadamu, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Sydney Ramadhani Mkumbi, ambaye katika makala hii amepata fursa ya kuelezea masuala mbalimbali yanayohusu jeshi hilo na historia ya maisha yake kama alivyofanya mahojiano mapema wiki hii na Mwandishi Wetu, Happiness Katabazi.

Swali: Ni kitu gani kilikusukama hadi ukajiunga na Jeshi la Polisi?

Jibu:
Ukakamavu waliouonyesha askari wa kike walipofika kutembelea Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora mwaka 1960. Jinsi walivyokuwa wanatembea, hata walivyokuwa wanajieleza mbele ya kadamnasi, walinivutia sana.

Swali: Wewe kama mama wa familia unawezaje kumudu kazi ya jeshi na familia?
Jibu: Kupanga ni kuchagua. Kazi yoyote utakayoifanya bila kupanga huwezi kuimudu. Hivyo wakati wa kazi ni kazi kweli, na familia ina muda wake wa kuiangalia. Hata hivyo namshukuru mume wangu aitwaye Ramadhani Mkumbi, ambaye naye pia ni Ofisa wa Polisi, kuwa ni mwelewa na ni mvumilivu, anathamini kazi yangu na amekuwa bega kwa bega nami kwa kila ninachokifanya, namshukuru sana.

Swali: Inasemekana kwamba nafasi za kujiunga na jeshi hivi sasa ni lazima uwe na kigogo akukingie kifua ndipo upate nafasi. Unalizungumziaje hili?


Jibu: Siyo kweli, binafsi naelewa kwamba kuna ushindani mkubwa katika kujiunga na Jeshi la Polisi hivi sasa. Kwa sababu watu wengi wanapenda kujiunga na jeshi na nafasi ni chache. Aidha, kuna masharti ambayo yameainishwa kwa waombaji. Wakiyatimiza wanateuliwa.

Swali: Kuna wasichana uraiani wanapenda kazi ya jeshi, lakini wamejaribu kutafuta kazi hiyo hawajafanikiwa unawashauri nini wasichana hawa?

Jibu: Kama wana elimu inayohitajika na kama wanatimiza masharti kama vile urefu wa futi 5 nchi 3 na miaka isiyozidi 25 wasikate tamaa. Aidha waepukane na makundi ya uovu bali wawe karibu na Jeshi la Polisi kufichua maovu.

Swali: Unafikiri idadi ya wanawake waliobahatika kupata uongozi ndani na nje ya jeshi wanatosha, na kama hawatoshi nini kifanyike?

Jibu: Hawatoshi. Na tuliobahatika kupata uongozi tuonyeshe kumudu vema madaraka yetu. Na hao walio nyuma yetu waonyeshe uwezo ili viongozi wetu na serikali kwa ujumla wazidi kuwa na imani na utendaji kazi wetu.

Swali: Wewe ni askari mwanamke mwenye cheo cha juu kuliko askari wanawake ndani ya Jeshi la Polisi nchini, unafikiri askari wa kike waliojiunga na jeshi katika karne ya 21 ni tofauti na askari wa kike ukiwemo wewe mmoja wao mliojiunga na jeshi hilo katika karne ya 20?

Jibu
: Tofauti iliyopo kati ya askari waliojiunga karne ya 20 na hii karne ya 21 haiwahusu askari wa kike tu, bali askari wote kwa sababu askari wengi waliojiunga katika karne ya 20 walijiunga kwa wito, hivyo wanaipenda kazi yao na kuifanya kwa uadilifu. Tofauti na wa karne ya 21 ambao baadhi ya wameingia kukidhi haja ya ajira tu.

Swali: Unafikiri idadi ya wanawake waliobahatika kupata uongozi ndani na nje ya jeshi wanatosha na kama hawatoshi nini kifanyike?

Jibu:
Awali ya yote niishukuru serikali iliyomo madarakani kwa kutambua umuhimu wa jinsia na kusema kweli maeneo mengi yaliyopewa wanawake kuongoza, wameonyesha umahiri wa uongozi. Hivyo basi tuliopewa nafasi ya uongozi tuitumie vizuri ili iwe kivutio/hamasa na kigezo kwa serikali kuendelea kutupa uongozi.

Swali: Binafsi tueleze jambo lililowahi kukutokea ambalo hutalisahau katika maisha yako?

Jibu: Nakumbuka kati ya mwaka 1976/1977 nikiwa Mwendesha Mashitaka Mahakama ya Mkoa wa Dodoma mbele ya aliyekuwa Hakimu wa Mkoa Mh. Kajeri, alimhukumu mtuhumiwa mmoja (jina nalihifadhi) kwenda jela miaka mitatu kwa kosa la unyang’anyi wa kutumnia nguvu na mara baada ya mahakama kwisha mtuhumiwa alimrukia mlalamikaji na kumkaba koo nusura amtoe roho, ndipo nilipovua kiatu aina ya gongo na kumtwanga nacho sehemu ya hatari (pressure point) na kumfanya aone giza na kumnusuru mlalamikaji. Nina sisitiza sitalisahau tukio hili.

Swali: Imekuwa ikidaiwa kwamba ndani ya majeshi yetu askari wa kike wamekuwa wakinyanyaswa kijinsia na askari wanaume, unalizungumziaje?

Jibu:
Binafsi, nakubaliana kabisa na wewe kwamba miaka ya nyuma sisi askari wa kike tulikuwa tukinyanyaswa sana na askari wanaume kwa sababu tulikuwa na mipaka ya kufanya kazi kwa mfano ilikuwa si rahisi kumkuta askari wa kike akifanya kazi wilayani, ilikuwa tunafanyia kazi makao makuu ya mkoa tu.
Lakini hivi sasa wanaume hawatunyanyasi kwa kuwa tunajua haki zetu hivyo tunafanya kazi nao sambamba.

Swali: Unazungumziaje mwaka mmoja wa utawala wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema?

Jibu: Isitoshe tu kusema kwamba pamoja na mambo mengine, serikali kutambua umuhimu wa kuunda wizara inayoshughulikia mambo ya kipolisi, kuwepo na uwezo zaidi wa kiuchumi serikalini.

Wananchi kutambua matatizo yanayoikabili idara hasa baada ya uhalifu wa kimataifa kuibuka nchini ghafla na la muhimu zaidi Inspekta Jenerali wa Polisi wa sasa kuwahi kufanya kazi Shirikisho la kimataifa la Jeshi la Polisi (Interpol) kumemsaidia kuleta ubunifu na maboresho zaidi katika jeshi letu ili liwe la kisasa.

Mabadiliko katika Jeshi la Polisi yanachangiwa na mkakati wake wa ulinzi shirikishi na ulinzi jirani ambao umesaidia kuliweka Jeshi la Polisi kuwa karibu na wananchi, hivyo wananchi wamejitokeza kutoa taarifa za uhalifu.
Mwisho, lakini si katika umuhimu, mabadiliko katika Jeshi la Polisi yanachangiwa na kaulimbiu ya serikali ya Awamu ya nne ya Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya, nayo yamesaidia mahitaji ya polisi ambayo hayakuwepo hapo nyuma kupatikana.

Swali: Wewe ni miongoni mwa askari wanawake wachache ndani ya Jeshi kuteuliwa kuwa mkuu wa kitengo cha makosa dhidi ya binadamu yakiwamo makosa ya mauaji, ubakaji na malalamiko, unadhani unapewa ushirikiano wa kutosha na askari wanaume?

Jibu: Ninapewa ushirikiano mkubwa sana na wanaume kwani watendaji kazi wakuu wengi wao ni wanaume.

Swali: Lini umeteuliwa kuwa mkuu wa kitengo cha makosa dhidi ya binadamu?
Jibu: Niliteuliwa kuwa mkuu wa kitengo hicho mwaka 2004 ambapo hadi sasa nakiongoza kitengo hiki.

Swali: Ni changamato gani zinakikabili kitengo chako unachokiongoza?

Jibu: Kama mkuu wa kitengo cha makosa dhidi ya binadamu, changamoto ambayo inanikabili katika kitengo hiki hasa ni pamoja na ucheleweshaji wa upelelezi hususan makosa ya mauaji, ubakaji na kadhalika, hivyo kusababisha mlundikano wa mahabusu magerezani na hata malalamiko kuwa mengi kana kwamba kwa sababu uchunguzi umekwama, basi mtuhumiwa anadai kubambikiwa kesi.
Hivyo kama mkuu wa kitengo ninalazimika kuwahimiza wakuu wa upelelezi wa mkoa kusimamia upelelezi na wakati mwingine kufanya semina kukumbushana/kuelimishana na wakati mwingine kukemea ucheleweshaji wa upelelezi wa makosa ya jinai kwa ujumla na athari zake.

Swali: Ni askari wanawake wangapi kwa sasa wana cheo kama chako cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)?

Jibu: Kwa sasa ni mwanamke peke yangu ndiye mwenye cheo hiki cha (SACP), na ninaweza kusema mimi ni mwanamke wa tano kushika cheo hiki kwani tayari hapo nyuma kulikuwa na maofisa wanawake wanne ambao wamestaafu kwa muda tofauti walikuwa na cheo hiki cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi.


Swali: Tupatie siri ya mafanikio yako hadi ukakikwaa cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) kwa kuwa ni nadra mno kwa askari wa kike kupata cheo hicho?

Jibu: Ukweli wanawake ni wachache, sana ambao tumefikia cheo hiki cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na siri ya mafanikio yangu hadi kufikia hapa nilipo ni kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na kufuata taratibu zote zilizopo katika jeshi letu ikiwa pamoja na kuwatii viongozi wangu na kutekeleza maagizo/amri halali ninazopewa.
Aidha, niwashukuru kwa dhati kabisa wazazi wangu Bwana na Bibi Nathaniel Mpena (ambao wote ni marehemu “Mungu awaweke mahali pema peponi)’ ambao walinilea katika maadili ya dini na kunisimamia hadi kupata elimu ambayo ilikuwa adimu kwa wanawake wa wakati ule.

Swali:Tupatie takwimu za makosa ya binadamu ambayo umewai kuyapokea na yakafanyiwa kazi?

Jibu:
Nisikufiche, kwasasa siwezi kukutajia idadi kamili ya makosa ya binadamu kwani makosa yanayoletwa hapa ni mengi mno. Ila ninachokumbuka mwaka 2006 mimi nilikuwa ni Mwenyekiti wa Tume ya Polisi ya kumhoji aliyekuwa Kamanda wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam, ACP- Abdallah Zombe, na wenzake 12, wanaokabiliwa na tuhuma za mauaji ya watu wanne ambao ni wafanyabiashara ya madini na wakazi wa Mahenge mkoani Morogoro, ambao kabla ya mimi kuongoza tume ya kuwahoji, Tume ya Rais ya kuchunguza mauaji ya watu hao iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Kipenga Mussa, ambayo tume hiyo baada ya uchunguzi wake ilibaini kwamba wafanyabiashara wale hawakuwa majambazi kama ilivyokuwa imedaiwa awali na Jeshi la Polisi.

Swali: Naomba kufahamu historia ya maisha yako kwa mapana.

Jibu: Mimi ni mtoto wa tano katika familia ya watoto saba kwa mzee Nathaniel Mpena, mzaliwa wa Kijiji cha Lukula wilayani Sikonge, Tabora. Nimesoma Shule ya Msingi Iwensato II, kati ya mwaka 1958-1960. Shule ya wasichana ya kati Usoke, na mwaka 1961-1964 nilijiunga na kuhitimu Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora mwaka 1965-1968.
Nilipohitimu shule Februari 18, 1969 nilijiunga rasmi na Jeshi la Polisi katika Chuo cha Polisi (CCP) Moshi na kufanya kazi mikoa mbalimbali ikiwemo CCP Moshi, Dodoma, Mtwara, Kilimanjaro na Makao ya Polisi Idara ya Upelelezi.
Aidha, nimefanya kazi mbalimbali ikiwa pamoja na uendeshaji wa mashitaka ambao naweza kusema kwamba robo tatu ya maisha yangu katika Jeshi la Polisi nimekuwa mwendesha mashitaka katika mahakama za mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro.
Nimeolewa, nina watoto watano, wa kwanza anaitwa Hussein (35), huyu anafanya kazi Umoja wa Mataifa (UN), Kulwa na Dotto (32), Adili (35) ambaye kwa sasa yupo masomoni Poland, Bahati (18), ambaye ni mtoto wa kike pekee niliyemzaa, na kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Loyola.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0755 312 859, barua pepe: katabazihappy@yahoo.com au www.katabazihappy.blogspot.com.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili la Juni 17,2007

3 comments:

 1. Mwandishi,
  Asante kwa makala nzuri. Ila kuna makosa kadhaa umefanya katika kuandika. Kwa harakaharaka niseme kuwa Adili hana miaka 35. Pia Bahati si mtoto wa kike ila wa kiume. Kama utaweza kurekebisha hilo itakuwa vema. Vinginevyo nampa hongera sana dada yangu Sydney kwa kazi na juhudi yote hadi hapo alipofika. Kama mwanamke/mama ilikuwa ngumu sana.

  Ng'wana Itimba.

  ReplyDelete
 2. Your method of explaining evеrything іn this parаgraρh is
  аctually good, all be сapаble of effortlessly know it, Thanκs
  a lot.

  my page ... buy best stairlift

  ReplyDelete
 3. Naona umri umeenda kwa maelezo yalivyo. Bado umo jeshini ?

  ReplyDelete