Mwelekeo wa Taifa Sasa Taabani

Na Happiness Katabazi

NATUMAINI wasomaji wote ni wazima wa afya. Nisiwachoshe, leo nitaanza makala yangu kwa kuandika nukuu moja ya muasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere.

Nukuu hiyo inapatikana miongoni mwa hotuba zake maarufu, katika kitabu kiitwacho ‘Moyo kabla ya silaha’, aliyoitoa mwanzoni mwa miaka ya 1960. Na nitaichambua kwa mapana.

Jifunze wakati ni huu: “Afadhali tuwe na taifa ambalo halina silaha za kisasa, lakini tuna moyo wa ushujaa, kuliko kuwa na taifa lenye silaha, lakini vijana wake ni waoga. Tuwe taifa la binadamu, tujue wapi tunatoka na wapi tunakwenda.

“Kuwa na moyo safi ni jambo jema sana kwani tukiwa na moyo safi silaha zitafuata baadaye. Afadhali kuwa maskini, lakini tunajitegemea, kuliko kuwa matajiri kwa kuomba na kutegemea taifa jingine. “Tujiamini kwa nguvu zetu zote na tunajitegemea. Taifa linaloshiba makombo siyo taifa hata.

“Tuwe na tabia ya ushujaa, tusiwe waoga. Tuwe na tabia ya kujitegemea na kusaidiana. Ni afadhali kuwa na chakula kidogo, lakini tukagawana kidogo kidogo kuliko kuwa na chakula kingi na tukaanza kukigombea. Tanzania iwe na tabia mpya. Inawezekana, timiza wajibu wako.”

Aya ya kwanza ya nukuu hiyo Mwalimu Nyerere, alikuwa anaona kwamba vijana wengi walikuwa wanadai wapewe silaha, watakomboa taifa na kukomboa Bara la Afrika kutokana na ukoloni na ubeberu.

Hasa wakati huo vita ya uhuru ilikuwa inarindima katika nchi za Msumbiji, Angola, Zimbambwe na kwingineko.

Nchi hizo zilikuwa chini ya ukoloni na ubeberu na Tanzania ilikuwa makao makuu ya kamati ya ukombozi ya Afrika ya Umoja wa Nchi Uhuru za Afrika.
Na wakati huo ndege za Wareno zilikuwa zikivuka mpaka na kudondosha mabomu nchini mwetu.

Mwalimu Nyerere aliona upungufu katika mtazamo wa vijana wale kwamba silaha ndiyo njia sahihi ya kukomboa ukoloni na ubeberu.

Yeye aliona ni tofauti, kwani alichokuwa anakihitaji yeye ni commitment, uwe unaliamini hilo jambo kwa moyo wako wote na akili zako zote na ujitoe mhanga kulitetea Bara la Afrika. Hiyo ndiyo nadharia ya upambanaji na huo ndio msingi wa upambanaji.

Mwalimu alizungumzia katika mazingira hayo. Je, leo hii kauli hiyo inatugusa vipi Watanzania, umma ambao idadi kubwa ya Watanzania ni vijana? Na je, tuna amini kwa moyo wote kuhusu vita dhidi ya ubeberu? Ukweli ni kwamba hatuamini.

Walio wengi hawaamini kama kuna ubeberu, wanaamini kwamba kuna utandawazi kwa maana kwamba mtaji wa kibeberu unaweza ukatumika kulikomboa taifa na kufuta umaskini.

Kwa Watanzania wengi wa leo wanatofautiana sana na Mwalimu Nyerere, hawana moyo wala ushupavu wa kupambana na ufisadi, rushwa na mtaji wa kibeberu nchini. Na kwa hakika sera nzima ya uwekezaji ni tamko la kukumbatia ubeberu.

Kwa msingi huo vijana hawana budi kupambana na hata kuhitaji kuwa na moyo wa ushujaa. Tumeishakubali kwamba wageni wana haki kubwa hata kuliko wananchi kuwekeza na kuvuna rasilimali zetu.

Wajibu wetu na nafasi tuliyonayo ni kuomba ajira. Na katika hilo hakuna cha ushupavu wala cha woga, cha msingi ni kumpigia magoti na kumlamba miguu tajiri ili upate mradi wako.

Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba ili tuwe na taifa la binadamu linalostahili heshima lazima tujue wapi tunatoka na wapi tunakwenda: Kwa hilo Watanzania wa leo hatumo kwa sababu hatuna sera.

Tunachokiabudu leo hii ni kupewa misaada na wafadhili ambao sasa ndio wanatupangia mipango yetu na uchumi wa maendeleo. Kazi kubwa ya watendaji wa serikali ni kuandika michanganuo (proposals) ili kupewa fedha, na kweli kazi hiyo ya watumishi wa serikali inafanikiwa na kila wanapopewa pesa inafuatia kazi kubwa (shokoa) ya kuandika ripoti na kuwapelekea wakubwa waliotoa fedha zao kwa nchi yetu.

Mwalimu Nyerere alisema, afadhali kuwa maskini, lakini tunajitegemea kuliko kuwa matajiri kwa kuomba kutegemea taifa jingine, kwa maana hilo taifa linalostahili heshima ni lile linalojiamini, linalotegemea nguvu zake kwa maendeleo yake badala ya taifa linaloshiba ‘makombo’ linayopewa kwa jina la misaada.

Hebu tujiulize, Tanzania tunajitegemea kwa kitu gani? Vijana wetu hawajui tena kilimo wala hawapendi ufugaji, kwa hiyo chakula kilicho sokoni na kwenye supermarket kinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Na hawapendi kwa sababu hakuna mazingira mazuri yatakayowashawishi wakijikite kwenye sekta hiyo.

Tanzania haina tena viwanda vya nguo, japo inazalisha pamba. Tanzania haisindiki kahawa wala matunda japo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao hayo. Tanzania haizalishi mafuta ya kula, inanunua mafuta hayo kutoka nje ya nchi ambazo nyingine ni jangwa japo Tanzania inazalisha zao la alizeti, karanga na mbegu nyingine za mafuta ya kula.

Viwanda vyetu tunaviuza, tena kwa wingi, vingine vinafungwa na vilivyopo ni vya jua kali vinavyozalisha bidhaa duni zisizo na tija wala thamani kwenye masoko ya kitaifa na kimataifa.

Kwa mantiki hiyo, Tanzania sasa ni jalala la kila kitu, kuanzia mitumba na kila uchafu unaotoka nje hasa nchi za Asia.

Je, kwa staili hii ni kiburi gani tunaweza kuwa nacho wakati tumeshindwa kujitegemea kwa kila kitu? Cha msingi nikuona jinsi taifa letu lilivyo taifa la waoga kiuchumi, kwani badala ya kuanzisha miradi ya kuzalisha mali, tunaanzisha miradi ya uchuuzi ya kuuza karanga na takataka kutoka nje.

Kwetu maendeleo ya uchumi ni kuligeuza taifa kuwa la wachuuzi wa aina ya wamachinga. Sasa ujasiri gani tutakuwa nao wakati sote ni maskini wa mali, kauli, maadili na elimu na afya mgogoro?

Taifa la aina hii ni taifa duni ambalo litatugeuza kuwa taifa la watumwa wa mataifa mengine.

Sasa hivi Watanzania wamechoka hata kufikiri, wanaogopa kufikiri na wako tayari kufuta Utanzania wao ili angalau watawaliwe na Wakenya au taifa lolote linalopenda kututawala. Hiyo ndiyo dhima la Shirikisho la Afrika Mashariki.

Unapoona mtu anakwenda sokoni kwa mikikimikiki na makelele wakati hana fedha wala bidhaa anayokwenda kuiuza sokoni, basi ujue mtu huyo kama si ‘maaruni’ ni Mtanzania.

Wengi wa Watanzania wa leo ni watu wanaopenda kutumia njia za mkato zisizo sahihi, hawapendi kufanya kazi wakatoka jasho wanapenda sana starehe na kucheza (Ngwasumaa, mipasho) na matokeo ya taifa kuwa na watu kama hawa ni kuwa na taifa la matapeli, wasanii, wala rushwa, wapika majungu, mafisadi, wazandiki na watu wasioaminika kabisa na hii sasa imeanza kuwa sifa kuu ya Watanzania kimataifa.

Kwa hiyo hivi sasa ukikutana na Mtanzania awe rais, mbunge, viongozi, mawakili, wafanyabiashara, matajiri, walemavu na wananchi wa kawaida unaanza kuwa na wasiwasi kwamba huyo si mmoja mwenye sifa kama hizo nilizozitaja hapo juu.

Si siri tena, zile zama za Mtanzania ni kioo cha uadilifu duniani zimekwisha kabisa.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

0755 312 859: katabazihappy@yahoo.com au www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Juni 10,2007, ukurasa wa nane

2 comments:

  1. Hongera Happiness.

    Wewe ni Mzalendo Halisi.

    Tembelea blogu ya Mlenge kwa mchanganuo kuhusu Tanzania. http:/www.mlenge.blog.com

    ReplyDelete
  2. Happy asante ndugu na mungu akubariki tu dada yetu we. It's about time somebody say something. Tumekuwa tukiwacheka sana wa-West Africa na North Africa kuwa hawana mwelekeo wa maisha lakini sasa Tanzania ndio tunakoelekea at a speed of light, Mh sijui ndio mwisho wa hiki kizazi tena umefika.
    Anyway hongera sana Happy for the bogg. Good luck

    ReplyDelete